Friday, 24 July 2015


WASANII WATAKIWA KUFUATA TARATIBU WANAPOENDA NJE YA NCHI ILI KUEPUKA MATATIZO NA MIKANGANYIKO INAYOWEZA KUJITOKEZA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa nchini linawakumbusha wasanii wote nchini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo wanapokwenda nje ya nchi kufanya maonesho au kushiriki shughuli yoyote ya Sanaa ili kuepuka matatizo na mikanganyiko mbalimbali inayoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa taratibu zilizopo, msanii yeyote anapokwenda nje ya nchi anapaswa kujaza fomu maalumu inayotolewa na BASATA na baadaye kupewa kibali bure (bila gharama yoyote) ambacho mbali na kueleza wapi msanii anaelekea kinaeleza kwa kina tarehe ya kuondoka kwa msanii na ile ya kurudi nchini.

Kutokana na kukua kwa sekta ya Sanaa nchini hususan muziki na filamu wasanii wengi wamekuwa wakipata fursa ya kwenda nje ya nchi kufanya maonesho na shughuli zingine za Sanaa hivyo suala la kufuata sheria, kanuni na taratizu za kupata vibali vya kwenda nje ya nchi ni muhimu sana ili kuhakikisha kwanza; safari zao zinakuwa na baraka ya moja kwa moja kutoka Serikalini, pili kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za wasaniii wanaokwenda nje ya nchi, tatu usalama wa wasanii wetu na mwisho, kuwakabidhi bendera ya taifa kama ishara ya uwakilishi na ubalozi wa nchi yetu katika mataifa wanayoyatembelea.

BASATA limekuwa likiwaelekeza wasanii wote kuomba vibali vya kwenda nje ya nchi na kuripoti katika balozi zetu zilizoko kwenye mataifa mbalimbali ili kuhakikisha wanakuwa na wenyeji katika nchi husika kwa lengo la kujitambulisha pia kupata msaada pale kunapotokea tatizo lolote linalohitaji utatuzi wa Serikali.

Dunia imekuwa na matukio mengi ya kiusalama ni vema kuchukua tahadhari hasa ikizingatiwa kazi za Sanaa huambatana na mikusanyiko mikubwa ya watu hali ambayo inaweza kuzaa matatizo kwa wasanii wetu wakiwa nje ya nchi bila kuwa na nyaraka stahiki.   

Baraza la Sanaa la Taifa linatambua kwamba wasanii wanapokwenda nje ya Tanzania kwa lengo la kufanya kazi ya Sanaa wanakwenda kuipeperusha bendera ya Taifa letu, kwa mantiki hii ni mabalozi wa nchi. Hivyo basi, lazima wawe wazalendo, wajivunie utanzania na kuiwakilisha vyema nchi yetu.

Ieleweke kwamba Serikali inafarijika na kupata heshima kubwa inapoona wasanii wetu wakivuka nje ya mipaka na kwenda kupata mafanikio kwenye majukwaa ya kimataifa suala ambalo ni kuitangaza Tanzania kupitia Sanaa na Utamaduni baada ya kuzingatia taratibu zote. Ndiyo maana kupitia mitandao yake ya kijamii na hata katika programu ya Jukwaa la Sanaa BASATA limekuwa likihamasisha wadau wa Sanaa kuwaunga mkono wasanii na kuwapigia kura kunapokuwa na shindano lolote linalohitaji ushindi wa kura (popular vote). Aidha, BASATA limekuwa likiandika taarifa kwenye vyombo vya habari kumpongeza msanii yeyote anapofanya vizuri nje ya mipaka ya nchi yetu.

Ni sababu hii ndiyo imelifanya BASATA muda wote kuwasisitiza wasanii na menejimenti zao kutambua wajibu wao kwa serikali hasa katika kuhakikisha wanafuata taratibu zote zilizopo na kutoa taarifa hitajika serikalini ili kuepuka mikanganyiko na sintofahamu inayoweza kujitokeza.

Lengo ni kuhakikisha kupitia taarifa sahihi zinazokuwa zimetolewa na menejimenti za wasanii au wasanii wenyewe pia kupitia taarifa zilizopo kwenye vibali vya kwenda nje kwa wasanii husika, Serikali nayo inajipanga ipasavyo katika kuhakikisha wasanii wetu wanaagwa na baadaye kupokelewa kwa heshima wanaporejea nchini.

BASATA linaamini kwamba haileti picha nzuri na kwa kweli inashusha morali wasanii wetu wanaporudi nyumbani na mafanikio makubwa pasi na mapokezi ya Kiserikali kwa sababu tu menejimenti za wasanii zinashindwa kujipanga kwa maana ya kuzingatia taratibu zilizopo na kutoa taarifa stahiki za lini msanii atarejea na wakati gani ili mamlaka husika ifanye utaratibu wa mapokezi.  

Serikali kupitia BASATA imefanya mapokezi stahiki kwa wasanii Peter Msechu aliposhinda shindano la Tusker Project Fame, Mtunzi wa filamu Timoth Konrad wakati filamu yake ya ‘Dogo Maasai’ iliposhinda tuzo nchini Marekani na hivi karibuni imefanyika kwa Msanii Mayunga aliyeshinda shindano la Airtel Tracing Star. Aidha, washiriki wote wa mashindano ya urembo wamekuwa wakifanyiwa hivyo kama ilivyo kwenye sekta ya michezo.

BASATA linatoa wito kwa wasanii kudumisha upendo baina yao na kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano pia mawasiliano ya karibu na Serikali muda wote kwani zipo mamlaka ambazo zipo kwa ajili ya kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika tasnia ya Sanaa.

Ni wazi kwamba kama wadau wote wa sanaa wakielewa utaratibu huu basi sekta ya Sanaa ambayo kiasili ni ya upendo, mshikamano na amani itaendelea kukua katika mwenendo mwema na kuwa yenye tija zaidi kwa wasanii wenyewe pamoja na jamii kwa ujumla. Wasanii tudumishe upendo, amani na mshikamano.

Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Godfrey Mngereza

KATIBU MTENDAJI

No comments:

Post a Comment