Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha
Msanii wa muziki wa dansi Ramadhan Ally Masanja (Banza Stone) kilichotokea nyumbani
kwao Sinza jijini Dar es Salaam leo mchana siku ya Ijumaa ya tarehe 17/07/2015
baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Banza
Stone ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na
mchango mkubwa katika kukuza muziki wa dansi nchini hasa katika kubuni miondoko
mbalimbali ambayo ilikuja kupata umaarufu mkubwa. Moja ya mwondoko uliopata
umaarufu mkubwa ni ule wa “Achimenengule”
akiwa na Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT).
Mchango
wake katika muziki wa dansi hasa katika kubuni na kutunga nyimbo zenye ubora,
ujumbe na maadili kwa jamii hautasahaulika kamwe. Ni mwanamuziki aliyeacha misingi
katika sekta ya muziki na alijitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki
wa dansi mahali ulipo leo.
Itakumbukwa
kwamba mnamo Julai 3, 2015 BASATA na Asha Baraka, Mkurugenzi wa African Stars
Entertainment (ASET) walichukua juhudi za makusudi kwenda nyumbani kwa msanii
huyu kufanya mashauriano na familia yake ikiongozwa na kaka yake Khamis Ally
Masanja na hatimaye kwa pamoja kumrejesha tena hospitalini kwa ajili ya
matibabu yake.
Hata
hivyo pamoja na juhudi hizo za kupigania uhai wake Mungu kampenda zaidi Msanii mwenzetu
Banza Stone. Upendo wetu kwake umezidiwa na ule wa mwenyezi Mungu ambaye
kimsingi wote tutarejea kwake.
Baraza,
wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote
aliyotuachia marehemu Banza Stone hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi katika
kukuza muziki wa dansi na sekta ya muziki kwa ujumla.
Baraza
linatoa pole kwa ndugu wa marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote
wa Sanaa katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey
Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment