Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini
linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria,
kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia
muda wa matumizi ya kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum
hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu.
Aidha,
BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni marufuku
kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ ili
kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu
unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa
wakijisahau na kutamani kutengeneza faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa
disko kwa watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa ambayo
yangedhibitika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA
kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisitiza kwamba
halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu
maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha
maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayekiuka maagizo haya.
BASATA
linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Eid El Fitr na yenye furaha tele.
Sanaa
ni kazi, tuipende na kuithamini.
Godfrey
Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment