BASATA KURUDISHA HADHI YA MUZIKI WA REGGAE
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae
Production House iliyo chini ya Msanii Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa
limeandaa programu maalum kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae
nchini.
Programu hiyo ambayo itafanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala
Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa
4:00 hadi saa 6:30 Mchana kupitia Programu ya Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi
kwa ajili ya kuurudisha muziki wa reggae jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki
huu na kuja na mikakati bora ya kuurudishia hadhi yake.
Ieleweke kwamba katika siku za karibuni muziki huu wa reggae umekuwa umeganda
na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa
burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama
Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawe na wengineo.
Changamoto kubwa si tu ni muziki huu kutochezwa kwenye vyombo vya
habari bali pia kuna changamoto ya wasanii wenyewe kutokubadilika na
kutengeneza muziki unaokwenda sambamba na soko pia hitaji la mashabiki.
Ni nia ya BASATA kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini
wanahudhuria programu hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatma ya
muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na
kuburudika Jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu.
BASATA linaamini kwamba baada ya programu hii wasanii wa reggae na
wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa
reggae nchini na kuhakikisha unaendelea kudumu.
Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na kuithamini
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA
No comments:
Post a Comment