Timu
ya watendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ikiongozwa na Kaimu Katibu
Mtendaji wa Baraza hilo Bi. Vivian Nsao Shalua mapema jana imemtembelea Msanii
na mwimbaji wa muziki wa Bendi ndugu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone” ambaye kwa sasa
amekuwa akiugua nyumbani kwao maeneo ya Sinza
Jijini Dar es Salaam.
Lengo
la ziara hii ilikuwa kumjulia hali Msanii huyu mahiri wa Bendi na kushauriana
na familia yake juu ya namna bora ya kusaidia matibabu yake na kuhakikisha
anapata huduma zote stahiki kulingana na maelekezo ya daktari wake.
Katika
ziara hiyo, watendaji hao wakiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars
Entertainment (ASET) Mama Asha Baraka walipata wasaa wa kufanya mazungumzo na
familia ya mwanamuziki huyo ili kupata maendeleo ya afya yake, matibabu na
mwenendo wake.
Wanafamilia
hao wa Msanii Banza Stone wakiongozwa na Kaka yake Khamis Ally Masanja
walieleza kwamba hali ya mgonjwa huyo imekuwa ikibadilika mara kwa mara na kwamba
amekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Sinza iliyoko Sinza Palestina
jijini Dar es Salaam. Aidha amekuwa akipelekwa hospitali mbalimbali za Jiji la
Dar es Salaam kulingana na maelekezo ya daktari wake.
Baada
ya kupata taarifa ya kina kuhusu afya ya msanii Banza Stone, watendaji wa
BASATA kwa kushauriana na wanafamilia hao walifunga ziara kwenda hopitali ya
Sinza kufanya utaratibu wa matibabu na kuhakikisha anapewa huduma ya stahiki
ili kuhakikisha afya yake inaimarika.
Akizungumza
hospitalini hapo Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA Bi. Shalua alitoa wito kwa
wadau wa Sanaa na wasanii kwa ujumla kumwombea msanii Banza Stone na kujitolea
kwa hali na mali katika kuhakikisha anarejea katika hali yake ya zamani na
hatimaye kurudi kwenye Majukwaa ya maonesho.
“Wadau
wa Sanaaa tumwombee msanii wetu. Msanii huyu ni muhimu kwenye tasnia ya muziki
wa dansi. Amechangia sana katika kukuza muziki huu hapa nchini. Tumwombee ili
arudi katika hali yake” amesisitiza Bi. Shalua.
Imetolewa na Kitengo cha Habari cha
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
No comments:
Post a Comment