Na
Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wameiomba
Serikali kumalizia ujenzi wa ukumbi wa Sanaa za maonesho unaojengwa kwa zaidi
ya miaka minane sasa makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) eneo la Ilala
sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo mapema wiki hii,
wasanii hao walieleza kwamba kwa sasa kuna ufinyu wa kumbi za za maonesho hali
ambayo imekuwa ikiwafanya wasanii hao kukosa maeneo ya kufanya sanaa zao hivyo
kumalizika kwa ukumbi huo itakuwa ni ahueni kubwa kwao.
“Ukumbi huu ni muhimu sana
kwetu, wengi tuliutazama kama mwanzo wa ufufuaji wa Sanaa za majukwaani lakini
sasa ni muda mrefu hauoneshi dalili za kumalizika. Kuna kila sababu ya ukumbi
huu kukamilika ili kutusaidia katika maonesho yetu” alisema Msanii Khalid
Kambau.
Kwa upande wake msanii wa
Sanaa za maigizo Christian Kauzeni ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha
wasanii waigizaji mkoani Dar es Salaam alisema kwamba kutokana na ukumbi huo
kutazamwa kama mkombozi wa wasanii kuna kila sababu ya kuangalia mbinu
mbalimbali ili kuhakikisha unakamilika mapema iwezekanavyo.
Awali akiwasilisha mada
kwenye Jukwaa hilo la Sanaa iliyohusu ‘Ubora wa Filamu na Changamoto zake’
msanii na mzalishaji filamu maarufu nchini William Mtitu alisema kwamba tasnia
ya filamu chini imepata umaarufu na kukua ingawa bado changamoto za uharamia,
elimu na masoko zimeendelea kuiathiri.
“Kwa sasa filamu
zinazozalishwa zimekuwa na ubora kuliko huko nyuma. Tatizo liko kwenye elimu
kwa wasanii, uharamia na masoko. Kulikuwa na maduka zaidi ya sabini na tano yanayouza
kazi za wasanii wa filamu lakini kwa sasa yamebaki sita tu. Wengi wameamua
kuuza kazi za nje mbazo ni nafuu. Hii ni hatari” alisisitiza Mtitu.
Aliongeza kwamba pamoja na
Serikali kuirasimisha sekta ya filamu bado kuna changamoto ya kazi zinazotoka
nje kutokuwekewa stempu za mamlaka ya mapato huku kukiwa na uharamia unaotishia
bei za filamu halali zenye stempu hizo.
Jukwaa la BASATA limekuwa
likifanyika kwa mwezi mara mbili siku za Jumatatu na wiki hii kulikuwa pia na
utambulisho wa asasi ya ubalozi wa Utamaduni wa Mwafrika ambayo imeasisiwa
nchini Cameroon, Afrika Magharibi mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment