Friday, 31 July 2015

YAH: KUFUNGIWA KWA MSANII ZUENA MOHAMED MAARUFU KAMA SHILOLE KUJISHUGHULISHA NA KAZI ZA SANAA KWA MUDA WA MWAKA MMOJA





Tarehe: 31/07/2015
  

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

BASATA Arts Centre                                                             Tel. 2863748/2860485
                                                                                              Fax: 0255- (022) – 286 0486                                                                                                                         
Ilala Sharif Shamba                                                                                                                                                                       
P.O. Box. 4779, Dar es Salaam
E-mail:basata06@yahoo.com

KUFUNGIWA KWA MSANII ZUENA MOHAMED MAARUFU KAMA SHILOLE KUJISHUGHULISHA NA KAZI ZA SANAA KWA MUDA WA MWAKA MMOJA.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015   hadi tarehe 24/07/2016.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015 akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya  wapenda sanaa za Tanzania na hivyo akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili.  

 Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na maadili awapo jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo yake kwa nini asichukuliwe hatua  za kinidhamu
kwa kitendo chake cha kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo.  Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya kazi ya sanaa  kwenye onesho lake la   huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria, Kanuni  na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.

Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005 limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja tokea tarehe 24/07/2015. 

Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.

Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

Wednesday, 29 July 2015

WASANII WAELEZWA UMUHIMU WA KUJIWEKEA AKIBA



Na mwandishi wetu;

WASANII nchini wametakiwa kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba katika mifuko mbalimbali ya jamii kwa kuwa kufanya hivyo kuna kumuhimu mkubwa katika maisha yao baada kuwa wamestaafu kazi zao au wanapokuwa hawana tena uwezo wa kufanya kazi.

Hayo yalisemwa na msanii mkongwe wa maigizo hapa nchini Bakari Mbelemba maarufu kwa jina la Mzee Jangala wakati akizungumza katika Jukwaa la na Sanaa lililofanyika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.

Mzee Jangala alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na msanii Christian Kauzeni ambaye alitaka kujua ni kwa nini wasanii wakongwe wengi wanakuwa na maisha magumu licha ya kuwa walifanya kazi nzuri zilizo wajengea umaarufu mkubwa hapa nchini.

Alisema wasanii wengi wakonge hawakuwa na utaratibu wa kuweka akiba, lakini kwa sasa kuna mifuko mingi na mifumo mingi ya kujiwekea akiba hivyo ni muhimu kwa wasanii kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza alisema huu si wakati wa msanii kupata shida baada ya kustaafu au kuzeeka kwa kuwa kuna mifuko mingi ya kuweka akiba na hata ya huduma za afya ambayo kwa mchango kidogo inatoa unafuu mkubwa wahuduma.
“Haipendezi kwa msanii aliyekuwa na jina kubwa au umaarufu katika nchi anapokuwa amepatwa na maradhi kusubili harambee ipite ili apate matibabu, msanii akijiunga na mfumo wa bima ya Afya kwa mfano NHIF analipa fedha kidogo sana na anapata uhakika wa matibabu kwa muda mrefu wa maisha yake,” alisema Mngereza.

 

Msanii mkongwe Mzee Jangala (kulia) akiteta jambo na mratibu wa jukwaa la sanaa Rajab Sollo katika jukwaa la nje jana. Kushoto ni mwenyekiti wa jukwaa hilo Bw. Ernest Biseko.



Wasanii wa kikundi cha Mandela Theater Group wacheza ngoma katika onyesho lao walilofanya kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika hivi karibuni katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).


Wasanii wa kikundi cha Mandela Theater Group wakifanya igizo  la uelimishaji katika Jukwaa la Sanaa lililofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).


 
 Matukio mbalimbali katika picha kwenye Jukwaa hilo...