Friday, 23 December 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.

Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi wa ukumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.

Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Christmas na Mwaka mpya ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.

Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.

BASATA mamlaka inayotoa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.

BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa Heri ya Christmas na Mwaka Mpya.

 

SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza  
KATIBU MTENDAJI, BASATA

 

Wednesday, 14 December 2016

JUKWAA LA SANAA BASATA PALIKUWA HAPATOSHI LEO



Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) limefanya program yake ya Jukwaa la Sanaa kwa wadau wa sanaa na wa kazi za sanaa.


Mada ya leo ilikuwa:
Fursa za Sanaa Kutokana na Mabadiliko ya Teknolojia na Dunia ya Utandawazi .

Mtoa mada:  
Ruge Mutahaba (Mfanyabiashara, mtunzi na mdau wa muziki).


Bw. Mutahaba; Alisema “Sanaa yetu ina mapato mengi kama serikali kupitia BASATA na mamlaka nyingine husika zikiamua kubadili mfumo uliopo na kujikita katika mifumo ya sanaa kwa maana ya kibiashara ili mbali na kukuza vipaji na vipato kwa wasanii mmoja mmoja lakini pia kuongeza pato la taifa”.


Pia amewashauri “Wasaani kutokana na mabadiliko ya teknolojia na dunia ya utandawazi, sanaa ni biashara kubwa kwasasa, hivyo tunapaswa kufahamu na kujua vizuri  kuchanganya vionjo mbalimbali vya utamaduni wetu wa Kitanzania ili kupata ladha inayouzika sokoni hata kimataifa”.


Aidha amewasihi wasanii kuzingatia na kuwa na weledi wa kutosha wa kutumia mitandao ya kijamii ili kuweza kujitangaza kiurahisi na kwa haraka lakini pia kufikisha kazi zao kwa jamii kubwa zaidi.





Ruta Maximilian Bushoke "Bushoke" naye alikuwpo akifatilia mjadala kwa makini kwenye Jukwaa la Sanaa


Mtendaji wa BASATA Bw. Kurwijira Maregesi Ng'oko akitoa ufafanuzi juu ya jambo fulani kwenye Jukwaa hilo.
Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Godfrey L. Mngereza akitoa ufafanuzi wa jambo fulani.