BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo
ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha wamiliki na
waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa
kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na
vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi wa ukumbi,
kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na
kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki
wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika
kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya
Christmas na Mwaka mpya ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za
sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuandaa madisko ya
watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata
sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji
wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya
vibali vyao, wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa
na BASATA.
BASATA mamlaka inayotoa vibali vya kumbi
za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote
utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye
kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali
na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote
wa Sanaa Heri ya Christmas na Mwaka Mpya.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment