Wednesday, 31 January 2018

TAARIFA KWA UMMA/VYOMBO VYA HABARI





UKWELI KUHUSU KUTOFANYIKA KWA FAINALI ZA ‘MISS TANZANIA 2017’

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limekua likifuatilia kwa umakini mwenendo wa shindano la Miss Tanzania na waandaji wake kampuni ya LINO Agency katika kuhakikisha taratibu, kanuni na miongozo ya kuendesha matukio ya Sanaa  nchini inazingatiwa.

 


Hivi karibuni LINO wametoa taarifa ya kutokufanyika kwa shindano Miss Tanzania kwa mwaka 2017 ambapo pamoja na sababu ya kukosa wadhamini wametaja kucheleweshewa kibali na BASATA kama sababu ya kutokufanyika kwa shindano hili kwa msimu wa mwaka 2017.

 


Tunapenda kueleza kwamba sababu inayotolewa na LINO kwamba walicheleweshewa kibali na BASATA si ya kweli na pengine imetengenezwa kuficha uhalisia wa changamoto za shindano hili ambazo mara zote BASATA na hivi karibuni Waziri mwenye dhamana na sekta ya Sanaa Mh. Dkt Harrison Mwakyembe amezieleza na kuzitolea maagizo.

 


BASATA kama mtoa vibali vya matukio ya Sanaa nchini limeshangazwa na taarifa ya kutokuwepio kwa shindano kwa msimu huu maana tayari lilikwishatoa kibali cha muda kwa kampuni ya LINO ili kufanya maandalizi ya awali ya shindano hili sambamba na kuandaa mshiriki wa shinda la Miss World 2017 lililomalizika hivi karibuni mji wa Sanya nchini China amabapo Tanzania tuliwakilishwa na mshiriki Julitha Kabete aliyekabidhiwa bendera chini ya uangalizi wa Wizara na BASATA. 

 


Kibali hicho cha muda ambacho kilitolewa mapema tarehe 08/09/2017 kinatoa fursa kwa mwandaaji wa tukio la Sanaa kufanya maandalizi yote ya awali ya tukio la Sanaa/Burudani huku akiwa chini ya uangalizi maalum wa kukamilisha taratibu mbalimbali za msingi kwa ajili ya kupewa kibali cha mwisho cha tukio husika hivyo kampuni ya LINO haina sababu yoyote ya kutaja kibali cha BASATA kama kikwazo cha kufanyika kwa shindano la Miss Tanzania mwaka huu maana tayari walikua na kibali hiki cha muda kinachowapa fursa za maandalizi yote ya awali ya shindano.

 


Tunazidi kutoa wito kwa waandaaji wote wa mashindano/matukio ya Sanaa kuzidisha weledi na zaidi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kuendesha matukio ya Sanaa kama zinavyo fafanuliwa katika vikao vya mashauri mara kwa mara. Aidha tunazidi kusisitiza umuhimu wa kujenga taswira chanya kwa matukio ya Sanaa na kuyajengea uendelevu ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuyapa mvuto mkubwa wa kibiashara.

 


BASATA kama msajili na mtoa leseni katika matukio ya Sanaa tutaendelea kuzingatia weledi na kutoa huduma zetu kwa haraka, ubora na kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa ambazo kwa pamoja wadau wote tumeziridhia.


“Sanaa ni Kazi”

KATIBU MTENDAJI


BARAZA LA SANAA LA TAIFA - BASATA

AHSANTE SANA MH. RAIS


SHEREHE ZA UHURU WA TANZANIA BARA 09/12/2017


PONGEZI

Kwa niaba ya wadau wa Sanaa na Watanzania kwa ujumla tunapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii @alikiba_page na @officialnandy kwa ushindi wa tuzo za #afrima2017 . Ushindi wao umeliletea taifa heshima na kuendelea kuuweka muziki wetu kwenye ulimwengu wa Sanaa #afrima2017 #pongezi #basata

 

SANAA NI KAZI

#EastAfricaArtBiennale

"Sanaa ni kazi kama ilivyo kazi nyingine, tuna kila sababu ya kuilinda, kuithamin na kuiendeleza sanaa hii ya uchoraji. 


Nimeona hapa kuna picha zina bei kubwa sana, lakini bei hii haimzuii mteja kuinunua kazi hii, kwani thamani na ubora wa kazi husika ndio unaofanya bei kuwa kubwa au ndogo.


Ndugu wasanii, Tanzania ya viwanda inakuja na muda si mrefu wachoraji wataanza kuhitajika kwa wingi zaidi kwenye viwanda kwenda kuchora viatu, magauni nk.

Lakini pia mbali na kutuinua kiuchumi, sanaa inatuunganisha kijamii watu wa tamaduni mbalimbali na mataifa mbalimbali leo tupo hapa kwa ajili ya sanaa hii.

Kama serikali tunapata fursa na mialiko mbalimbali kuhusu sanaa hii, hivyo nawashauri ndugu zangu wasanii tuje tujisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili tutambuane na tupate takwimu sahihi miongoni mwetu na hatimaye tuweze kugawana fursa hizi kiurahisi mara tu zinapojitokeza." Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Onesmo Kayanda. (Tarehe 06/11/2017 kwenye ukumbi wa Alliance Française - Dar es Salaam)







 

MH. WAZIRI AKUTANA NA WASANII

Picha na Dondoo za tukio la Waziri mwenye dhamana na Sanaa Dkt. Harrison Mwakyembe na Naibu wake Juliana Shonza walipokutana na Wasanii wa Fani zote tarehe 27/10/2017 kupitia programu yetu ya Jukwaa La Sanaa. Katika kikao hicho waziri ametolea majibu kero zifuatazo:

1. Suala la muda wa Wasanii wa Muziki katika maenesho yao ambapo kumekuwa na kubanwa muda na kulazimishwa kukatisha maonesho. Waziri amesema tayari ameshazungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na tayari kamati imeundwa kupitia sheria ndogo za manispaa zinazokwamisha.

2. Sheria ya hakimiliki na maboresho yake yako katika hatua za mwisho na ameeleza kwamba ni nzuri na itatatua matatizo ya wizi wa kazi za Wasanii.

3. Kuundwa kwa Idara za Sanaa katika halmashauri. Ameeleza ameshazungumza na Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI kuhusu suala hili na linafanyiwa kazi. Ameahidi kulitolea ripoti.

4. Amezungumzia wasanii kutokaa kimya wanapodhulumiwa haki zao. 
Amewataka kuanza kutumia TEHAMA katika kuuza kazi zao 
na kuepuka watu wa kati ambao wamekua wakifaidika zaidi yao. Ameeleza kufurahishwa na Shirikisho la Sanaa za Ufundi ambalo tayari limezindua mfumo wa TEHAMA katika kunadi na kuwafaidisha wasanii wa Sanaa za Ufundi.







TUZO ZA AFRIMMA 2017

Tunampongeza kwa dhati Msanii Naseeb Abdul aka Diamond Platnumz kwa heshima kubwa aliyotupatia Watanzania kwa kushinda tuzo ya AFRIMMA
Ndugu mdau wa sanaa.., msanii kama Diamond na wasanii wengine kwa ujumla wao ni hazina kubwa kwa taifa letu.
Je, unawashauri wafanye nini ili wavilinde na kuvikuza zaidi vipaji vyao?