Sunday 27 September 2015

BASATA KURUDISHA HADHI YA MUZIKI WA REGGAE



Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production House iliyo chini ya Msanii Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa limeandaa programu maalum kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini.


Programu hiyo ambayo itafanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:30 Mchana kupitia Programu ya Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi kwa ajili ya kuurudisha muziki wa reggae jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki huu na kuja na mikakati bora ya kuurudishia hadhi yake. 


Ieleweke kwamba katika siku za karibuni muziki huu wa reggae umekuwa umeganda na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawe na wengineo. 

 

Changamoto kubwa si tu ni muziki huu kutochezwa kwenye vyombo vya habari bali pia kuna changamoto ya wasanii wenyewe kutokubadilika na kutengeneza muziki unaokwenda sambamba na soko pia hitaji la mashabiki. 

 

Ni nia ya BASATA kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini wanahudhuria programu hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatma ya muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na kuburudika Jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu.


BASATA linaamini kwamba baada ya programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na kuhakikisha unaendelea kudumu.

 

Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na kuithamini

 


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA


Friday 25 September 2015

BASATA LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU




Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari hususan radio na runinga kuondoa na kuacha mara moja kurusha au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye maudhui ya kashfa, matusi, kejeli, udhalilishaji ambazo zinahatarisha kuigawa jamii ya kitanzania katika misingi yoyote hasa katika kipindi hiki Taifa linapoendelea na kampeni za kisiasa na kujiandaa na uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa kifungu namba 118 (a-d) cha Sheria ya Bunge namba 9 ya Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka 2010 ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza, kuzalisha, kusambaza au kutangaza ujumbe ambao una mlengo wa matusi, dharau, uzushi au jinai kwa lengo la kutukana, kutisha, kusumbua au kushusha hadhi ya mtu mwingine.

Aidha, Sheria ya Bunge namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 45 (1) (a-c) kinatoa mamlaka kwa taasisi au mtu yeyote anayebaini uvunjifu wa Sheria katika mitandao kutoa notisi kwa yeyote yule anayesambaza au kutangaza ujumbe au maudhui yanayovunja sheria za nchi kuacha mara moja au vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayekaidi.

Ni kwa msingi huu, BASATA linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na wale wenye akaunti kwenye mitandao ya kijamii kama sound cloud, U-Tube, ITunes nk. kuondoa ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya kwanza ya taarifa hii nyimbo zote zinazokengeuka maadili na kubeba mlengo wa matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji wa watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa na kitaifa.

Aidha, BASATA linawakumbusha tena Wasanii wote nchini kuacha mara moja kubuni na kutengeneza kazi za Sanaa zenye kuashiria kuigawa jamii katika misingi yoyote ya kibaguzi na zaidi kutumia Sanaa kubomoa jamii badala ya kuijenga.

BASATA linawasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari hususan radio na runinga pia watangazaji na Ma DJs kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza maudhui yoyote ya Sanaa yenye mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na mgawanyiko wa Taifa.

BASATA kwa mamlaka yake chini ya Sheria namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta na Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa kushirikiana na vyombo vya dola halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari ambavyo vitaendelea kutangaza na kusambaza nyimbo zenye mwelekeo wa kuhatarisha usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.

BASATA likiwa ni msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua kwamba Sanaa ikitumiwa kwa ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha machafuko, mivurugano na kupotea kwa amani nchini. Hivyo umakini unahitajika miongoni mwa wasanii katika kuzingatia weledi, maadili, uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama chombo cha kujenga jamii yenye kuzingatia maadili.  

SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI

Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA

BASATA KUURUDISHA MUZIKI WA REGGAE JUKWAANI



Tuesday 1 September 2015

MWASITI AWATAKA WASANII WABADILIKE, WAZINGATIE MAADILI WAWAPO JUKWAANI



Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Mwasiti Almas amewataka wasanii wenzake kuwa wabunifu katika kutanua mianya ya kujiingizia kipato na kuhakikisha wanazingatia maadili wawapo jukwaani ili kulinda hadhi zao.

Mwasiti ameyasema hayo mapema wiki hii wakati akijibu maswali ya wadau wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwa mwezi mara mbili ziku za Jumatatu makao ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala Sharif Shamba.

Wadau hao wa Sanaa walitaka kujua ni kwa nini wasanii wengi hufilisika mara wanaposimama kufanya shughuli za Sanaa na wengine wamekosa ubunifu wawapo kwenye maonesho au wanapozalisha kazi zao hali ambayo inawafanya watumie sehemu za siri za miili yao katika kutafuta mvuto kwa mashabiki.

“Wasanii wengi wanang’ang’ania kwenye sanaa pekee. Hawawekezi kwenye miradi mingine. Kuwa na umaarufu si kuwa na fedha bali umaarufu ni njia tu inayokusaidia kuingia kwenye sekta na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiimarisha kimapato” alisema Mwasiti wakati akifafanua suala la wasanii kufilisika mara wanapochuja kwenye Sanaa.

Alizidi kueleza kwamba wasanii waliopo sasa hawana budi kutambua kwamba hawatakuwepo muda wote bali kuna leo na kesho hivyo lazima kuiandaa kesho sasa.
“Umri wa wasanii unaenda, waliopo sasa hawawezi kuwepo kesho kwani kuna wasanii wengi wanaibuka na lazima wapate nafasi. Ni muhimu sana kwa wasanii kuliona hili. Huko nyuma kaka na dada zetu walipata shida ilikuwa ngumu lakini kwa sasa wasanii tunapata kipato na baadhi wanajitahidi kuwekeza” alisema Mwasiti.

Kuhusu wasanii kufanya maonesho yasiyo na maadili, Mwasiti alisema kwamba inasikitisha sana kwani katika hali ya kawaida msanii anayejitambua na kuthamini utu na hadhi yake hawezi akafanya maonesho ya uchi kwani matendo ya wasanii huathiri sana jamii inayowazunguka.
“Matendo yetu wasanii huathiri sana jamii inayotuzunguka. Sisi ni binadamu na tuna leo na kesho. Sipendi siku zijazo watoto wetu waje kuuliza na kushangaa yale tuyafanyayo sasa maana yataendelea kuonekana” alisema Mwasiti.

Katika Jukwaa hilo BASATA lilimwalika Mwasiti na wa msanii mwenzake wa kike Princes Dalyna anayefanya muziki wa reggae ili kueleza historia, changamoto na mafanikio waliyoyapata katika kazi zao za Sanaa.    

       Msanii wa Reggae Princes Delyla akiongea na wadau wa Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii kwenye makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Msanii Mwasiti Almas na Afisa Sanaa kutoka BASATA Augustino Makame.

       Msanii wa kizazi kipya Mwasiti Almas akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linalofanyika makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Msanii wa reggare Princes Dalyla na Afisa Sanaa kutoka BASATA Augustino Makame.

      Mtafiti na Msanii wa Reggae Innoncent Nganyagwa akifafanua jambo kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kulia kwake ni Msanii mwenzake wa Reggae Princes Delyla. 

       Msanii Mwasiti akisakata muziki sambamba na mashabiki wake kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA.

       Msanii Princes Dalyla akitoa burudani kwa wadau wa Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii

     Sehemu wa wadau wa Sanaa waliohudhuria Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifuatilia kwa makini burudani.