Na
Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wametakiwa
kurejesha kwa jamii sehemu ya faida wanayoipata kupitia kazi zao za Sanaa kwa
kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum ili kujijengea mtandao wa kudumu wa
masoko, uhalali na taswira nzuri kwa jamii.
Wito huo umetolewa mapema
wiki hii na mtengeneza filamu wa Tanzania mwenye makazi yake nchini Marekani
Bi. Honeymoon Mohamed wakati akiwasilisha mada kuhusu Filamu za Kitanzania na Masoko
kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA).
“Wasanii wanaitegemea jamii
kama chanzo cha mapato yao hivyo ni lazima wajenge utamaduni wa kurejesha kile
kidogo wanachokivuna kutoka kwa jamii kupitia kusaidia watu wenye uhitaji
maalum” alisema Honeymoon ambaye filamu yake ya Daddy’s Wedding imeshinda
tuzo kwenye tamasha la kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF) lililomalizika
hivi karibuni eneo la Ngome Kongwe, Zanzibar.
Aliongeza kwamba watoto
wenye uhitaji maalum wanapata faraja na kuhisi kupendwa na jamii pale
wanapotembelewa mara kwa mara na watu mbalimbali wenye umaarufu na nafasi kubwa
katika jamii hivyo wasanii wetu hawana budi kuwa sehemu ya kujenga faraja hii
kwa watoto hawa.
Kwa mujibu wa Honeymoon
wasanii wa Tanzania wako nyuma katika kuikumbuka jamii hususani kutembelea
makazi ya watoto wenye uhitaji maalumu na kuchangia huduma mbalimbali zinazokuwa
zinahitajika.
“Watoto wenye utindio wa
ubongo wako wengi, kuna wale wenye ulemavu wa ngozi na wengine wanaishi wakiwa
yatima kwenye vituo mbalimbali lakini wasanii wetu wamekuwa wazito kuwakumbuka.
Wasanii hawana budi kuyakumbuka makundi haya maana wako kwa ajili ya jamii”
alisisitiza.
Awali kabla ya uwasilishaji
wa mada hiyo, watoto wanaoandaliwa kupitia programu ya BASATA ya ‘Sanaa kwa
Watoto’ kutoka Shule ya Msingi wa Msimbazi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam
walitoa burudani mbalimbali za Sanaa wakisaidiana na Kikundi cha Sanaa cha
Jivunie chenye maskani yake neo la Mbagala Manispaa ya Temeke.
No comments:
Post a Comment