Thursday 27 April 2017

DR. MWAKYEMBE AKUTANA NA KAMATI YA MISS TANZANIA




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) tarehe 25 Aprili, 2017 amekutana na Kamati ya Miss Tanzania katika ofisi ya Wizara, Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw. Hashim Lundenga aliongozana na Katibu wake Bw. Bosco Majaliwa na Mjumbe Bw. Deo Kapteni. Mwenyekiti wa kamati alimuelezea Mhe. Mwakyembe kuhusu fursa na changamoto ambazo wamekutana nazo kwenye uandaaji wa mashindano hayo ya ulimbwende hadi sasa. Mhe. Mwakyembe ambaye aliambatana na Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Godfrey Mngereza na Mwanasheria wa Wizara Bw. Evod Kyando aliishukuru  Kamati kwa kumtembelea ofisini na pia kwa mchango wa muda mrefu kwenye tasnia ya ulimbwende nchini. Mhe. Mwakyembe alitoa rai kwa Kamati kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazohusu tasnia hiyo ya sanaa na kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanyika kwa mashindano ili kuepuka malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na washiriki kwa muda sasa. Mhe. Mwakyembe aliiagiza BASATA kuendelea kusimamia kwa ukaribu  maandalizi ya mashindano yote ya urembo na pale ambapo maandalizi yanasuasua wasisite kuchukua hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment