BASATA
LAPIGA MARUFUKU DISCO TOTO, KUMBI ZISIZO NA VIBALI.
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini limepiga
marufuku kumbi zote za burudani zisizo na vibali kufanya maonesho ya aina
yoyote.
Aidha, BASATA linawakumbusha
wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani wenye vibali kufuata sheria,
kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Katika
hili BASATA linawaelekeza wamiliki na mameneja wa Kumbi zote nchini kuhakikisha
wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa
utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi
ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu.
Aidha,
BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni marufuku
kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ ili
kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu
unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi za Eid El Fitr wamiliki na
mameneja hawa wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kumezwa na faida katika biashara
zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa
makubwa ambayo yangeweza kuepukwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA
mamlaka inayotoa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba
halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na
kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale
yanayoonesha maungo ya ndani.
Hatua
kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA
linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Eid El Fitr yenye
furaha tele.
Sanaa
ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey
Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment