Friday, 29 April 2016

BASATA KUAZIMISHA SIKU YA MUZIKI WA JAZZ DUNIANI





Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Elimu na Sayansi (UNESCO) litaungana na wasanii mbalimbali nchini na wadau wa Sanaa kuazimisha siku ya muziki wa Jazz duniani ambayo kwa mara ya kwanza itaazimishwa nchini Mei 2, 2016.
Maazimisho hayo ambayo yatapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wasanii wa muziki wa jazz hususan Band maarufu ya Das Jazz yanatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ofisi za BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Sambamba na burudani hizo, kutakuwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wadau wa muziki huu wa jazz ambazo zitalenga kuamsha ari, thamani na ufahamu wa muziki huu maarufu duniani miongoni mwa wasanii nchini.
Wawasilishaji wa mada hizo pamoja na mada zao kwenye mabano ni pamoja na John Kitime (Matumizi ya neno Jazz), Carola Kinasha (Uhusiano kati ya Elimu ya Muziki na Jazz) na Kurwigira Mareges (Historia ya Muziki wa Jazz) na Masoud Masoud (Ujue Muziki wa Jazz).
Mbali na burudani na mada hizo kuhusu muziki huo wa Jazz kutakuwa na wageni waalikwa kutoka kwenye balozi na vituo vya Utamaduni vya nchi mbalimbali zilizopo hapa Tanzania                
BASATA linatoa wito kwa wasanii na wadau wa muziki huu wa jazz kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya ambayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka sambamba na mataifa mengine duniani. 
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini


Godfrey Mngereza
Katibu Mtendaji – BASATA

No comments:

Post a Comment