Na
Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni
Ndugu Paul Makonda amelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kujali
afya za wasanii kufuatia kuandaa semina maalum kwa ajili ya kuwaelimisha wasanii
umuhimu wa kuwa na bima ya afya.
Akizungumza mwishoni mwa
wiki hii kwenye ufunguzi wa semina hiyo ya siku moja iliyofanyika kwenye Ukumbi
mpya wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba, Makonda alisema kuwa pamoja na BASATA
kuratibu sekta ya Sanaa limeona ni vema wasanii kulinda afya zao na kuhakikisha
wanakuwa na afya njema kupitia kuwa na bima ya afya.
“Nawapongeza sana BASATA kwa
kuona umuhimu wa afya kwa wasanii wetu. Kumbe pamoja na kuratibu sekta ya Sanaa
na kukusanya mapato kutoka kwenye kazi za Sanaa BASATA wanauona umuhimu wa afya
kwa wasanii” alisema Makonda.
Aliongeza kwamba katika
siku za hivi karibuni wasanii wamekuwa wakiombaomba fedha kwa ajili ya matibabu
ama kutatua matatizo mbalimbali hali ambayo inatokana na wao kutojiwekea akiba
ya fedha ili iweze kufaa katika kutatua changamoto hizo.
“Ni fedheha kubwa kwa
wasanii tena wengine maarufu kuombaomba kwa ajili ya matibabu. Lazima watokane
na aibu hii kwa kujiwekea akiba ya fedha kupitia mfuko wa Bima ya afya. Hili
litamaliza kabisa tatizo la wasanii kukosa fedha za matibabu” alisema Makonda.
Aidha, Makonda alieleza
kushangazwa na kukosekana kwa wasanii wengi maarufu
kwenye semina hiyo na
kueleza kwamba wao ndiyo wamekuwa ombaomba wakubwa pale wanapokuwa na shida ya
matibabu na wengine wamefikia hatua ya kuomba hata fedha za pango.
“Nashangaa sana katika
semina hii muhimu baadhi ya wasanii wakubwa siwaoni. Wanajiona wakubwa lakini
wao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuombaomba pale wanapokuwa na tatizo la
matibabu na hata kodi za nyumba wanazoishi” alieleza Makonda.
Awali akimkaribisha Mkuu
huyo wa Wilaya, Katibu Mtendaji wa BASATA Ndugu Godfrey Mngereza alisema kwamba
BASATA limeandaa semina hiyo kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) baada ya kuona wasanii wamekuwa na tatizo la kugharamia matibabu na
wamekuwa ni wa kutembeza bakuli pale wanapougua.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ndugu Paul
Makonda akimkabidhi kadi ya Bima ya Afya Katibu wa Shirikisho la Sanaa za
Ufundi Ndugu Godfrey Ndimbo
|
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu Paul
Makonda akiwa na viongozi wa mashirikisho ya wasanii nchini mara baada ya
kuwakabidhi kadi zao za Bima ya Afya.
|
Msanii Bakari Mbelemba maarufu kwa jina la
Mzee Jangala akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wasanii waliohudhuria semina
hiyo.
|
Sehemu ya umati wa Wasanii waliohudhuria
semina hiyo ya wasanii iliyofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA unaondelea
kujengwa.
|