BASATA
LAWATAKA WASANII KUWA TAYARI KUKOSOLEWA
Na
Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) limetoa wito kwa wasanii kuacha tabia ya kulewa umaarufu na kuchukia
pale wanapokosolewa kwani kazi yoyote ya Sanaa lazima ikosolewe ili iwe bora na
yenye kuvutia.
Wito huo umetolewa mapema
wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Godfrey Lebejo Mngereza wakati
akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA linalofanyika kwa mwezi mara mbili
siku ya Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba jijini
Dar es Salaam.
Alisema kuwa wasanii
wafurahie wanapokosolewa kwani msanii yeyote duniani lazima atenge muda wa
kuiwasilisha kazi yake kwa hadhira kwa ajili ya kusikilizwa au kuangaliwa na
hatimaye kukosolewa na kutolewa mawazo ya wadau kabla haijaenda sokoni rasmi.
“Kukosolewa kwa msanii ni
sehemu ya kazi. Wasanii wengine hulipa fedha nyingi kwa ajili ya kukosolewa na
kuboreshewa kazi zao. Hapa kwetu wasanii wanakosolewa bure, wanakasirika,
wanamwona adui anayewakosoa” aliongeza Lebejo.
Awali wakiwasilisha mada iliyohusu
Umuhimu wa msanii kutumia umaarufu
kukuza pato kwa nyakati tofauti kwenye Jukwaa hilo, mbunifu wa mavazi
maarufu nchini Asia Idarous and mwanamitindo Jokate Mwegelo kwa pamoja
walisisitiza umuhimu wa wasanii kuwa na malengo, bidii, uaminifu na kutengeneza
kazi zenye ubora.
Jokate alisema kwamba amefika
hapo alipo kutokana na kuzingatia uhusiano mwema katika kazi, kujitangaza,
kujituma, kujiwekea akiba na kujenga mtandao mzuri wa kikazi na wadau
mbalimbali ndani na nje ya nchi pia kujenga umaarufu mzuri usiyo na maadili
mabovu.
“Kupata umaarufu si kwa
mteremko. Si kila umaarufu ni mzuri. Wasanii lazima wabuni kazi nzuri na zenye
maadili ili zionekane na kupendwa. Tusibuni vitu vibaya au sisi wenyewe
kujinadi kwa vitu vibaya” alisisitiza Jokate.
Alizidi kueleza kwamba
hakuna kitu cha muhimu kwa msanii kama uvumilivu , kuepuka makundi yasiyo na
tija na zaidi kuwa karibu na watu wenye mafanikio katika kazi zao ili kuiga
yale yaliyo bora kwa ajili ya kukuza uchumi na pato.
Habari katika picha.
No comments:
Post a Comment