Na
Mwandishi Wetu
Baadhi ya wasanii nchini
wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kufikiria kupunguza au kufuta kabisa
ushuru wa forodha unaotozwa kwenye vifaa vya muziki wanavyoagiza kutoka nje ili
kukuza Sanaa na kusaidia mamilioni ya vijana ambao wamejiajiri kupitia sekta
hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya
wasanii mapema wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) mmoja wa wasanii anayeunda kundi la muziki wa kizazi kipya la Weusi Nick
wa Pili alisema kwamba, kwa sasa sekta hiyo ni kimbilio la ajira kwa vijana
wengi kwa hiyo Serikali haina budi kupunguza kodi kwa zana mbalimbali
zinazotumiwa na wasanii ili kurahisisha uzalishaji, kukuza tija na uchumi.
“Wasanii wengi kwa sasa
wanakwenda kufanya video na kutengeneza muziki nje ya nchi. Hii inatokana na
teknolojia yetu kuwa chini ya wenzetu. Naamini Serikali ikipunguza kodi katika
vifaa hivi na kuwawezesha wataalam tulionao basi nchi zote jirani zitakimbilia
kwetu” alisema Nick
Aliongeza kwamba vipaji vya
wasanii vipo vingi lakini kutokana na uzalishaji duni wa kazi za muziki na hata
filamu wasanii wamejikuta wakishindwa kushindana ipasavyo nje ya nchi na mara
nyingi kutumia gharama kubwa katika kufuata teknolojia hizo za juu nchi za nje
na hivyo kuikosesha serikali mapato.
“Wasanii wanakwenda kulipa
zaidi ya milioni arobaini kwa video moja tu nje ya nchi, hizi fedha zinakwenda
kukuza uchumi wa nchi zingine. Naamini kama Serikali ikijenga mazingira mazuri
ya kiteknolojia na zaidi kushusha gharama hizi basi nchi yetu itafaidika zaidi
na Sanaa” alizidi kusisitiza Nick.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Mitaji na Misaada kwa wasanii kutoka BASATA Bi. Elineca
Ndowo alisema kwamba sekta ya Sanaa nchini inazidi kukua na hivyo lazima
wasanii nao wafikirie kufanya kazi kisasa na kwa kufuata taratibu zote ili
kuipa serikali uhakika katika kupanga kulingana na hali halisi.
“Sekta ya Sanaa inakua,
lazima tuisaidie Serikali kuipa takwimu sahihi na moja ya njia ya kuhakikisha
hili ni kwa wasanii kujisajili, kusajili kazi zao na kuhakikisha taarifa sahihi
na kwa wakati zinapatikana. Hili litarahisisha upangaji wa mipango” alisema Bi.
Ndowo.
Jukwaa la Sanaa la BASATA
ni programu ambayo hufanyika kwa mwezi mara mbili siku ya Jumatatu na hutumika kama
jamvi la kuwaelimisha wasanii na kuwakutanisha kwa pamoja katika kubadilishana
uzoefu na mawazo kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sekta yao.
Msanii G Nako kutoka Kundi la muziki wa
kizazi kipya la Weusi akiimba sambamba na msanii mchanga ambaye hakufahamika
mara moja kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii.
|
Mdau huyu wa Sanaa naye hakuwa nyuma. Aliuliza
sababu za Wasanii wengi wa kizazi kipya kupenda kutumia playbacks badala ya
kuimba live Jukwaani.
|
Msanii anayechipukia kwenye tasnia ya filamu
kutoka taasisi ya mafunzo ya TAMAP akiwauliza maswali mbalimbali wasanii wa
kundi la Weusi kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii.
|
Picha, habari na Aristides Kwizela,
Afisa Habari wa BASATA.