|
|
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G.
Mwakyembe (Mb) tarehe 25 Aprili, 2017 amekutana na Kamati ya Miss
Tanzania katika ofisi ya Wizara, Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw.
Hashim Lundenga aliongozana na Katibu wake Bw. Bosco Majaliwa na Mjumbe
Bw. Deo Kapteni. Mwenyekiti wa kamati alimuelezea Mhe. Mwakyembe kuhusu
fursa na changamoto ambazo wamekutana nazo kwenye uandaaji wa mashindano
hayo ya ulimbwende hadi sasa. Mhe. Mwakyembe ambaye aliambatana na
Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Godfrey Mngereza na Mwanasheria wa Wizara
Bw. Evod Kyando aliishukuru Kamati kwa kumtembelea ofisini na pia kwa
mchango wa muda mrefu kwenye tasnia ya ulimbwende nchini. Mhe. Mwakyembe
alitoa rai kwa Kamati kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazohusu
tasnia hiyo ya sanaa na kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanyika
kwa mashindano ili kuepuka malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na
washiriki kwa muda sasa. Mhe. Mwakyembe aliiagiza BASATA kuendelea
kusimamia kwa ukaribu maandalizi ya mashindano yote ya urembo na pale
ambapo maandalizi yanasuasua wasisite kuchukua hatua zinazotakiwa kwa
mujibu wa sheria.