Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
lenye dhamana ya kufufua, kukuza na kuendeleza Sanaa nchini linapenda kuchukua
nafasi hii kumpongeza msanii na mbunifu wa Mavazi Mustafa Hassanali kwa kushiriki
kinyanga’anyiro cha Tuzo ya Mavazi ya Afrika Mashariki Kenya 2016 (Kenya
Fashion Awards 2016) yaliyofanyika tarehe 03/09/2016 na kupata tuzo ya Mbunifu
Bora wa Mwaka wa Afrika Mashariki.
Baraza linathamini mchango mkubwa wa
Mbunifu huyu wa mavazi katika kuendeleza tasnia ya ubunifu, kwa kuanzisha
Jukwaa la mavazi Afrika Mashariki na Kati, Swahili Fashion week na maonyesho
mengine ya mavazi.
Aidha tuzo hii itakuwa chachu kwa
ustawi wa tasnia ya ubunifu wa mavazi kwa kuwa imedhihirisha ubora wa kazi za sanaa
za Kitanzania katika soko la Kimataifa. Baraza litaendelea kushirikiana na
wabunifu wenye maono na bidii katika kukuza na kuendeleza sanaa nchini ili
kuhakikisha sekta ya sanaa inasonga mbele kwani ni ukweli usiopingika kuwa
tasnia ya sanaa ina mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa watanzania wengi
hususan vijana.
Baraza linatambua mchango wa Bwana
Mustafa Hassanali katika kukuza maendeleo ya ubunifu na amekuwa akitoa fursa
kwa wabunifu wengine wa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Baraza
linathamini na linatoa pongezi kwa Bwana Mustafa Hassanali kwa kazi nzuri
anayoifanya.
No comments:
Post a Comment