Wednesday, 6 July 2016

BASATA LAPIGA MARUFUKU DISCO TOTO, KUMBI ZISIZO NA VIBALI.



BASATA LAPIGA MARUFUKU DISCO TOTO, KUMBI ZISIZO NA VIBALI.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini limepiga marufuku kumbi zote za burudani zisizo na vibali kufanya maonesho ya aina yoyote.

Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani wenye vibali kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.

Katika hili BASATA linawaelekeza wamiliki na mameneja wa Kumbi zote nchini kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu.

Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.

Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi za Eid El Fitr wamiliki na mameneja hawa wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kumezwa na faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa ambayo yangeweza kuepukwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

BASATA mamlaka inayotoa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. 

Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.

BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Eid El Fitr yenye furaha tele. 

Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI