Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha
na Elimu na Sayansi (UNESCO) litaungana na wasanii mbalimbali nchini na wadau
wa Sanaa kuazimisha siku ya muziki wa Jazz duniani ambayo kwa mara ya kwanza
itaazimishwa nchini Mei 2, 2016.
Maazimisho
hayo ambayo yatapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wasanii wa muziki wa
jazz hususan Band maarufu ya Das Jazz yanatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa
Baraza hilo ulioko Ofisi za BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Sambamba
na burudani hizo, kutakuwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wadau wa
muziki huu wa jazz ambazo zitalenga kuamsha ari, thamani na ufahamu wa muziki
huu maarufu duniani miongoni mwa wasanii nchini.
Wawasilishaji
wa mada hizo pamoja na mada zao kwenye mabano ni pamoja na John Kitime
(Matumizi ya neno Jazz), Carola Kinasha (Uhusiano kati ya Elimu ya Muziki na
Jazz) na Kurwigira Mareges (Historia ya Muziki wa Jazz) na Masoud Masoud (Ujue
Muziki wa Jazz).
Mbali
na burudani na mada hizo kuhusu muziki huo wa Jazz kutakuwa na wageni waalikwa
kutoka kwenye balozi na vituo vya Utamaduni vya nchi mbalimbali zilizopo hapa
Tanzania
BASATA
linatoa wito kwa wasanii na wadau wa muziki huu wa jazz kujitokeza kwa wingi
katika maadhimisho haya ambayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka sambamba na
mataifa mengine duniani.
Sanaa ni kazi,
tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
Katibu Mtendaji – BASATA