Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani
nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata
sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa
kumbi.
Wanaelekezwa
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia
muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa
makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha,
BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni
marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko
Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Pasaka ili kuepuka maafa yanayoweza
kujitokeza.
Uzoefu
unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa
wakijisahau na kuendekeza faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa madisko
ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata
sheria, kanuni na taratibu.
Aidha,
baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi kwa msingi huohuo wa kuendekeza
faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao wamekuwa wakijaza watu kupita
viwango vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.
BASATA
kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba
halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na
kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha
maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayekiuka maagizo haya.
BASATA
linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa Pasaka njema na yenye furaha tele.
SANAA NI KAZI TUIKUZE,
TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA