Wadau wa muziki wa reggae
nchini kwa kujengewa mazingira na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wameweka
mikakati ya pamoja ya kuhakikisha wanaurudisha jukwaani muziki huo na kuainisha
changamoto mbalimbali zinazoukabili.
Akizungumza mapema wiki hii
kwenye programu maalum iliyolenga kuujadili muziki wa reggae na kuja na
mikakati ya kuurudishia hadhi iliyoandaliwa na BASATA, Msanii mkongwe wa muziki
huo Innocent Nganyagwa alisema kwamba wasanii wa muziki huo kwa sasa
wamejipanga kuurudisha jukwaani muziki huo kupitia kufanya maonesho maeneo
mbalimbali nchini.
“Tumejipanga kufanya
maonesho ya muziki wa reggae katika mikoa mbalimbali nchini, tutakuwa na kundi
la wasanii ambao kazi yao itakuwa kufanya maonesho ya hisani na kuurudisha
jukwaani muziki huu ambao kihistoria ni muziki mama” alisema Innocent
Nganyagwa.
Aliitaja mikoa ambayo
maonesho hayo ya reggae yatafanyika kuwa ni pamoja na Mbeya, Ruvuma, Iringa,
Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na mingine ambayo maandalizi bado yanaendelea ili
kuhakikisha wanawafikia wapenzi wengi zaidi wa muziki huu ambao huko nyuma
ulipata kuwa na mvuto mkubwa.
Mikakati mingine iliyowekwa
ukiacha kufanya maonesho mbalimbali nchini ni pamoja na wasanii wa reggae
kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika kujitangaza, kuanza kuuza kazi zao
kupitia mitandaoni, kubuni kazi zenye ujumbe unaoendana na soko na kuacha
kuganda na falsafa ya reggae ni muziki wa ukombozi.
Awali wakibainisha
changamoto mbalimbali zinazoukabili muziki huo, wadau wengi walisema kwamba
muziki huu unasuasua kutokana na vituo vingi vya radio kuupa kisogo, watanzania
wengi kuuhusisha na imani za urasta kitu ambacho si sahihi na zaidi wadau
muhimu hasa makampuni ya biashara kutoujali katika ufadhili.
“Muziki huu wa reggae si wa marasta pekee,
bahati mbaya watu wengi wamekuwa wakiuhusisha na imani za kirasta. Hapana.
Muziki huu unafanywa na mtu yeyote na ni muziki kama ilivyo miziki mingine”
alisema Ras Bumijah Zinyongwa ambaye pia ni kiongozi wa taasisi ya Tanzania
Rastafarai Movement (TARAMO)