Friday, 23 October 2015
Sunday, 27 September 2015
BASATA KURUDISHA HADHI YA MUZIKI WA REGGAE
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production House iliyo chini ya Msanii Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa limeandaa programu maalum kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini.
Programu hiyo ambayo itafanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:30 Mchana kupitia Programu ya Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi kwa ajili ya kuurudisha muziki wa reggae jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki huu na kuja na mikakati bora ya kuurudishia hadhi yake.
Ieleweke kwamba katika siku za karibuni muziki huu wa reggae umekuwa umeganda na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawe na wengineo.
Changamoto kubwa si tu ni muziki huu kutochezwa kwenye vyombo vya habari bali pia kuna changamoto ya wasanii wenyewe kutokubadilika na kutengeneza muziki unaokwenda sambamba na soko pia hitaji la mashabiki.
Ni nia ya BASATA kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini wanahudhuria programu hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatma ya muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na kuburudika Jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu.
BASATA linaamini kwamba baada ya programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na kuhakikisha unaendelea kudumu.
Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na kuithamini
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA
Friday, 25 September 2015
BASATA LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji wa wavuti, tovuti na
vyombo vya habari hususan radio na runinga kuondoa na kuacha mara moja kurusha
au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye maudhui ya kashfa, matusi, kejeli,
udhalilishaji ambazo zinahatarisha kuigawa jamii ya kitanzania katika misingi
yoyote hasa katika kipindi hiki Taifa linapoendelea na kampeni za kisiasa na
kujiandaa na uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa kifungu namba
118 (a-d) cha Sheria ya Bunge namba 9 ya Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka 2010
ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza, kuzalisha,
kusambaza au kutangaza ujumbe ambao una mlengo wa matusi, dharau, uzushi au
jinai kwa lengo la kutukana, kutisha, kusumbua au kushusha hadhi ya mtu
mwingine.
Aidha, Sheria ya Bunge
namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 45 (1) (a-c) kinatoa
mamlaka kwa taasisi au mtu yeyote anayebaini uvunjifu wa Sheria katika mitandao
kutoa notisi kwa yeyote yule anayesambaza au kutangaza ujumbe au maudhui
yanayovunja sheria za nchi kuacha mara moja au vinginevyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayekaidi.
Ni kwa msingi huu, BASATA
linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na wale wenye akaunti kwenye
mitandao ya kijamii kama sound cloud, U-Tube, ITunes nk. kuondoa ndani ya siku
saba (7) kuanzia siku ya kwanza ya taarifa hii nyimbo zote zinazokengeuka
maadili na kubeba mlengo wa matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji wa watu wa
kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa na kitaifa.
Aidha, BASATA
linawakumbusha tena Wasanii wote nchini kuacha mara moja kubuni na kutengeneza
kazi za Sanaa zenye kuashiria kuigawa jamii katika misingi yoyote ya kibaguzi
na zaidi kutumia Sanaa kubomoa jamii badala ya kuijenga.
BASATA linawasisitiza
wamiliki wa vyombo vya habari hususan radio na runinga pia watangazaji na Ma
DJs kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza maudhui yoyote ya Sanaa yenye
mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na mgawanyiko wa Taifa.
BASATA kwa mamlaka yake chini
ya Sheria namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta na
Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa
kushirikiana na vyombo vya dola halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na
kinidhamu kwa wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari ambavyo
vitaendelea kutangaza na kusambaza nyimbo zenye mwelekeo wa kuhatarisha
usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.
BASATA likiwa ni msimamizi
na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua kwamba Sanaa ikitumiwa kwa
ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha machafuko, mivurugano na kupotea kwa
amani nchini. Hivyo umakini unahitajika miongoni mwa wasanii katika kuzingatia
weledi, maadili, uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama chombo cha kujenga
jamii yenye kuzingatia maadili.
SANAA NI KAZI TUIKUZE,
TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
Tuesday, 1 September 2015
MWASITI AWATAKA WASANII WABADILIKE, WAZINGATIE MAADILI WAWAPO JUKWAANI
Msanii mahiri wa muziki wa
kizazi kipya Mwasiti Almas amewataka wasanii wenzake kuwa wabunifu katika
kutanua mianya ya kujiingizia kipato na kuhakikisha wanazingatia maadili wawapo
jukwaani ili kulinda hadhi zao.
Mwasiti ameyasema hayo
mapema wiki hii wakati akijibu maswali ya wadau wa Jukwaa la Sanaa
linalofanyika kwa mwezi mara mbili ziku za Jumatatu makao ya Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) Ilala Sharif Shamba.
Wadau hao wa Sanaa walitaka
kujua ni kwa nini wasanii wengi hufilisika mara wanaposimama kufanya shughuli
za Sanaa na wengine wamekosa ubunifu wawapo kwenye maonesho au wanapozalisha
kazi zao hali ambayo inawafanya watumie sehemu za siri za miili yao katika
kutafuta mvuto kwa mashabiki.
“Wasanii wengi
wanang’ang’ania kwenye sanaa pekee. Hawawekezi kwenye miradi mingine. Kuwa na
umaarufu si kuwa na fedha bali umaarufu ni njia tu inayokusaidia kuingia kwenye
sekta na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiimarisha kimapato” alisema Mwasiti
wakati akifafanua suala la wasanii kufilisika mara wanapochuja kwenye Sanaa.
Alizidi kueleza kwamba
wasanii waliopo sasa hawana budi kutambua kwamba hawatakuwepo muda wote bali
kuna leo na kesho hivyo lazima kuiandaa kesho sasa.
“Umri wa wasanii unaenda,
waliopo sasa hawawezi kuwepo kesho kwani kuna wasanii wengi wanaibuka na lazima
wapate nafasi. Ni muhimu sana kwa wasanii kuliona hili. Huko nyuma kaka na dada
zetu walipata shida ilikuwa ngumu lakini kwa sasa wasanii tunapata kipato na baadhi
wanajitahidi kuwekeza” alisema Mwasiti.
Kuhusu wasanii kufanya
maonesho yasiyo na maadili, Mwasiti alisema kwamba inasikitisha sana kwani
katika hali ya kawaida msanii anayejitambua na kuthamini utu na hadhi yake
hawezi akafanya maonesho ya uchi kwani matendo ya wasanii huathiri sana jamii
inayowazunguka.
“Matendo yetu wasanii
huathiri sana jamii inayotuzunguka. Sisi ni binadamu na tuna leo na kesho.
Sipendi siku zijazo watoto wetu waje kuuliza na kushangaa yale tuyafanyayo sasa
maana yataendelea kuonekana” alisema Mwasiti.
Katika Jukwaa hilo BASATA
lilimwalika Mwasiti na wa msanii mwenzake wa kike Princes Dalyna anayefanya
muziki wa reggae ili kueleza historia, changamoto na mafanikio waliyoyapata
katika kazi zao za Sanaa.
Mtafiti na Msanii wa Reggae Innoncent
Nganyagwa akifafanua jambo kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) mapema wiki hii. Kulia kwake ni Msanii mwenzake wa Reggae Princes
Delyla.
|
Msanii Mwasiti akisakata muziki sambamba na
mashabiki wake kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA.
|
Msanii Princes Dalyla akitoa burudani kwa
wadau wa Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii
|
Sehemu wa wadau wa Sanaa waliohudhuria
Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifuatilia kwa makini burudani.
|
Subscribe to:
Posts (Atom)